“Kwa sasa, hakuna kazi ya wavulana wala wasichana, sote tunaweza”

Alice Nifasha ni mojawapo ya wasichana wanaofanya kazi ya kunyoa nywele za watu. Hapo zama za kale, Sanaa ya kunyoa nywele ilikuwa ikionekana kama kazi iliyotengewa wavulana tu. Tulipomkuta akiwa anafanya kazi, aliweza kutushuhudia namna alivyoanza Sanaa hiyo na faida aipatayo kutoka hapo. Alice Nifasha alitushuhudia tena changamoto tofautitofauti zilizomkumba wakati alipoanza kazi hiyo.

Ni kawaida, mtu anapoanza kufanya kinachomkereketa ili kujitunza kimaisha, lazima kuwe na vizuizi vya wanaotaka kumkata tamaa na kumrudisha nyuma. Ila suluhisho la yote, mara nyingi ni kutosikia watu kama hao ikiwa amejinusuru kupambania maendeleo yake alikadharika “Mvumilivu hula mbivu”.

Alice Nifasha ni mojawapo ya wasichana aliyekumbwa na changamoto kama hizo wakati alipokuwa akipambania kujifunza na kuwa mfanisi wa kunyoa nywele za watu. Alice Nifasha alizaliwa mkoani Karusi, Tarafani Shombo, Kijijini Kiryama. Leo anajulikana kama Kinyozi anayefanya vema kazi yake. Shikiriza ilimkuta sehemu ijulikanayo kama « Kw’i Komabu” iliyomo Kijijini Gasunu, Tarafani Giheta mkoani Gitega ambapo alikuwa anafanyia kazi ya unyoaji akiwa pamoja na Babake.

Inaonekana kama ajabu kukuta Baba na mtoto wake tena wa kike wakifanyia pamoja kazi ya kunyoa nywele za watu. Msichana huyo Kama alivyoshuhudia mwandishi wetu alipomkuta kazini, leo hakuna kazi ya wavulana wala wasichana bali wasichana walishaelevuka na kupigania kipato ili kuchangia katika familia. Ni bora msichana kabla hajaenda kuolewa, ajitafutie mtaji au kazi ya kufanya ili ajipatie heshima. Ndicho kitu muhimu kitakachomfurahisha mmewe na familia yake Kwa ujumla.

Tayari miaka miwili ilishamalizika Alice Nifasha akiwa anafanya kazi hiyo na wateja wanaushuhudia ustadi wake.

“Baba yangu alipoanza kunifundisha kufanya kazi hii ya kunyoa, majirani walikuwa wakinikata tamaa kwa kusingizia kuwa faida nitakayoipata ni kushika mimba eti hakuna msichana wa kutafutia hela kwenye genge (Ligala), alikadharika hiyo ni kazi iliyotengewa wavulana tu.”

Alice Nifasha na Babake kamwe hawakutega sikio hao watu, waliendelea mpaka leo wanafanya kazi hiyo. Kilichotarajiwa na watu hakijamfikia. Cha muhimu ni kuifanya kipaumbele kazi yake.

Namna Alice Nifasha alivyoanza Sanaa hiyo anayoichangia na Babake

Vénérand Ntibatumakamwe, mzazi wa Alice Nifasha anashuhudia namna alivyofikiria hiyo kazi na kuamua kuirithi watoto wake.

“Kwanza Mimi muda mrefu nilikuwa ninafanyia mkoani Cibitoke, tarafani Buganda. Kabla ya kufikiria kazi hii, nilikuwa nimebanwa na vibarua nikitumikia watu wengine kazi tofautitofauti. Kiumizacho sana, kazi ilikuwa kama tembo ila mshahara sungura. Familia yangu ilikuwa inazidi Kuwa pana halafu nikajiwaza eti hapa kweli nitaweza kuitunza familia yangu na wakati uzee uko mlangoni?

Basi nikasema hebu nitafute fursa ya kufunzwa kunyoa halafu nirudi nyumbani. Baada ya fursa hiyo kupatikana na kufikia lengo langu, maisha yalianza kubadilika polepole kulingana na kipato nilichokuwa ninakipata. Basi nikaanza kukariri utofauti wa maisha ya kabla na ya wakati huo nikiwa Kinyozi.”

Vénérand Ntibatumakamwe alipokuwa Buganda hakufikiria kubaki huko. Alianza kanunua Vifaa mbalimbali kwa kusudi la kurudi nyumbani kama inavyosemwa kuwa “Nyumbani ni nyumbani hata kama ni chini ya mti”.

Vénérand Ntibatumakamwe alipofika nyumbani Kiryama, tarafani Shombo haikuwa rahisi kufanya kazi ya kunyoa bila umeme. Ilimpasa kununua sola na kutumia umeme wa sola ili kuendelea kazi vizuri.

Maisha aliyoyaishi mkoani Cibitoke, Vénérand Ntibatumakamwe anashuhudia tena somo aliloachiwa na maisha ya kule hadi kufikiria kudumisha kazi ya kunyoa na kuirithi watoto wake ikiwemo na Alice Nifasha.

“Niliporudi nyumbani kuendelea kazi hiyo na kuona kipato kinachopatikana niliridhika sana. Kuanzia hapo, niliona bora nisiendelee kutumika pekee yangu ndipo nilianza kuwafundisha watoto wangu. Nilianza kumfundisha mvulana ambaye ni kifunguamimba, na hadi leo alishamiliki sehemu yake pekee tena anafanyia hapa karibu yangu. Baadaye niliwafundisha hawa wasichana Alice Nifasha na mwingine ambaye yuko shuleni. Hao sasa ndio huwa tunafanyia pamoja hapa uliponikuta leo au nyumbani”, chambilecho Ntibatumakamwe (Baba wa Alice).

Faida aipatayo Alice Nifasha kutoka sanaa hiyo na wito anaotoa kwa wasichana wengine

“Tukiwa tunafanya kazi hii ni kama tuko shambani kulima. Kila tunachokipata huchangia nyumbani. Mama na watoto wengine wadogo hubaki katika shughuli zingine za nyumbani. Pesa tunazozipata hutumika kwa mahitaji ya nyumbani. Kwa upande wangu sikosi chochote, nikihitaji kununua simu, vocha Ama vitu vingine, pesa hutoka hapa. Baba hanyimi chochote japo hela hazipatikani kwa kiwango sawa kila siku. Kwa mfano katika kipindi cha siku kuu twaweza kupata angalau elfu 8 sarafu za Burundi kila mmoja, ila katika kipindi cha kawaida hupatikana kiasi cha pesa ambacho kiko kati ya elfu 4 na 5 sarafu za Burundi”, chambilecho Alice.

Alice Nifasha anatoa wito kwa wasichana wengine kutopuuzia kazi yoyote ile:

“Kila siku kutakuwa na wapinzani ila ushujaa unapiganiwa. Bila shaka kushika mimba isiyotarajiwa kamwe haitokani na kazi unayoifanya bali ni tabia ya mtu. Kwa mfano Mimi muda haunirahisishii kuwa kwenye genge ya wavulana. Lengo la mtu ndiko muhimu maishani mwake. Kwa upande wangu, Ikiwa hakuna wateja wengi ninatimiza majukumu mengine ya nyumbani”.